Tuesday, 25 October 2011

PICHA NA HABARI KUHUSU BASI LA DELUX LILILOUNGUA KWA MOTO

Raia walio wema wakijitolea kutoa maiti zilizoteketea kwa moto










Na hii ni video ya sehemu ya taarifa ya habari TBC, 
inayoosimulia kuhusu ajali ya basi la Deluxe

Abiria takriban 40 wanahofiwa kuteketea moto baada ya basi la Kampuni ya Deluxe Coach, walilokuwa wakisafiria kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma kupinduka na kulipuka moto.

Kwa mujibu wa watu walioshuhudia ajali hiyo, ilitokea jana saa tisa alasiri, eneo la Misugusugu, mjini Kibaha, mkoani Pwani, katika barabara kuu ya Morogoro. Imeelezwa watu 17 wamejeruhiwa.

Wameeleza basi hilo likiwa katika mwendo kasi baada ya kupandisha mlima liliyumba mara kadhaa, upande wa kushoto na kulia na baadaye lilipinduka.

Imeelezwa gurudumu la mbele lilipasuka, hivyo kuwa chanzo cha basi hilo kupoteza mwelekeo na kuanza kuyumba, kabla ya kupinduka na kuwaka moto, “Tuliona basi likiyumba, lilikwenda kushoto, baadaye kulia na liliporudi kushoto lilipinduka na papo hapo tukaona moto mkubwa, sijui nimeokokaje. “Nilikuwa nimekaa siti namba J4 na abiria mwingine niliyekutana naye ndani ya basi pale Ubungo, mpaka sasa karibu nusu ya abiria wameteketea moto,” alisema Shadrack Kobonga, abiria wa basi hilo.

Alisema walipandisha mlima wa Kongowe na walipopita kituo cha ukaguzi wa magari yanayoenda nje ya nchi, eneo la Misugusugu waliona gari limekuwa jepesi.

Scolastica Ponela, aliyeshuhudia ajali hiyo, alisema alikuwa njiani akitoka Ruvu kwa gari lingine, na walipokaribia eneo la ajali waliona moshi mzito, hivyo kushindwa kuendelea na safari, “Ilibidi tusimamie, tulishuka kwenye gari kwa kuwa haikuwezekana kupita, kulikuwa na moto, moshi ulitanda barabara yote. Tulielezwa kuna basi linaungua pamoja na abiria  waliokuwemo ndani,” alisema.

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga, athibitisha kutokea ajali hiyo, ingawa hakuweza kueleza idadi ya waliokufa.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ernest Mangu, alisema watu 17 wamejeruhiwa na ndio walionusurika katika ajali hiyo.

Alisema hawezi kusema idadi ya watu waliokufa kwa wakati huo (jana jioni) kwani wanaendelea na ufuatiliaji ili watoe taarifa kamili.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza, alishindwa kueleza lolote kuhusu ajali hiyo akisisitiza kwamba hali ni mbaya, “Siwezi kuzungumza lolote, nipo hospitali ya Tumbi, mpigie RTO na RPC sina la kusema hali ni mbaya,” alisema alipozungumza kwa njia ya simu.

No comments: