Wednesday, 24 April 2013

Serikali yafungia viwanda vya nondo - Dar


Dar es Salaam, Shirika la Viwango Tanzania (TBS), limevifungia viwanda viwili vya kuzalisha nondo kwa muda usiojulikana.

Viwanda vilivyofungiwa ni vya Metro Steel Mills kilichoko Vingunguti Dar es Salaam na Quaim Steel Milis kilichopo Chang’ombe wilayani Temeke.

Hatua hiyo imekuja baada ya kubainika kwamba vimekuwa vikizalisha na kuuza nondo zisizo na ubora wa viwango vinavyokubalika na hivyo kuwa tishio kwa watumiaji wa bidhaa hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Quaim, Hassan Amir, alisema kiwanda chake kilianza kuzalisha nondo tangu mwaka 2006.
Katika maelezo yake, , alipinga hatua hiyo ya TBS akidai kwamba inafanywa kinyume cha sheria, kwa madai kuwa hakupewa barua kabla ya amri ya kukifunga kiwanda chake.
Hata hivyo Mwanasheria wa TBS Baptista Bitao alisisitiza uhalali wa hatua hiyo, akieleza kuwa inafanywa kwa kuzingatia sheria inayompa mamlaka Inspekta wa shirika hilo kukifungia kiwanda kinachokiuka sheria ya viwango ya mwaka 2009.

“Hatua ya kusimamisha uzalishaji wa bidhaa ni ya kwanza kisha barua inatakiwa ifuate katika kipindi cha siku tatu, hawa wamefungiwa ili waweze kufuata utaratibu ikiwa ni pamoja na kuzalisha bidhaa zenye ubora, wakikiuka watawafikisha mahakamani,” alisema.

Meneja wa Kiwanda cha Metro, Onesmo Ngondo, alitoa lawama kwa TBS akidai kuwa haitoi elimu kwa wananchi na hasa wawekezaji, ili waweze kutambua umuhimu wa kupeleka bidhaa zao kuchunguzwa na kuthibitishwa kabla ya kuuzwa.

Akizungumzia kuhusu hatua hiyo, Ofisa Uhusiano wa TBS, Roida Andusamile alisema imetekelezwa baada ya TBS kuchukua sampuli ya vipande kadhaa vya nondo na kuvipima kwenye maabara yake.

Alisema katika uchunguzi huo, ilibainika kuwa nondo hazikuwa na ubora unaotakiwa.
Alisema hatua hiyo ya TBS ni mwendelezo wa kusaka bidhaa zinazozalishwa zikiwa chini ya kiwango.

Wiki iliyopita TBS ilianza kuzisaka nondo feki kwenye baadhi ya kampuni za usambazaji wa bidhaa hizo na kusimamisha uuzaji wa zaidi ya tani 1,350.
Hatua hiyo inafanywa chini ya ulinzi mkali wa polisi.
SOURCE: HABARI LEO

No comments: