Tuesday, 10 April 2012

TAARIFA KAMILI KUHUSU LULU

Elizabeth a.k.a Lulu
MSANII Elizabeth Michael ‘Lulu’ bado anashikiliwa Polisi na kuwa atafikishwa mahakamani upelelezi utakapokamilika kuhusu chanzo cha kifo cha msanii Steven Kanumba.
Lulu ndiye mtu pekee ambaye mpaka sasa anahusishwa na kifo cha Kanumba kilichotokea saa sita usiku wa kuamkia Jumamosi nyumbani kwake Sinza, Dar es Salaam.
Akizungumza jana Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alisema Polisi inaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha kifo hicho, ikiwa ni pamoja na kuchunguza mawasiliano ya simu.
“Inaonesha chanzo cha ugomvi wao ni wivu hasa kutokana na Lulu kutoka nje kwenda kuzungumza na simu, hivyo tunafanya uchunguzi wa mawasiliano ya simu na uchunguzi wa kisayansi kwa vielelezo vingine tulivyokuta eneo la tukio kama vile, mvinyo, soda na panga kama vilitumika.
“Pia tunasubiri ushahidi wa kitaalamu wa madaktari ambao muda huu (jana mchana) walikuwa wakiendelea na uchunguzi kubaini sababu za kifo katika hospitali ya Muhimbili.”
Kamanda Kenyela alisema kutokana na kosa lenyewe, Lulu hataruhusiwa kuhudhuria maziko ya Kanumba ambayo shughuli za kuaga mwili zitafanyika leo saa nne katika viwanja vya Leaders.
Kuhusu kufikishwa kwenye vyombo vya sheria, Kenyela hakutaja siku maalumu ya kufanya hivyo zaidi ya kueleza na kuwa atafikishwa kwenye vyombo vya sheria pindi taarifa zote muhimu zitakapokamilika.
“Siwezi kusema ni lini atafikishwa mahakamani kutokana na aina ya kosa lenyewe, tunataka tujiridhishe na kila upande upewe haki stahiki na tunataka kulitekeleza hili mapema zaidi. Ninachoweza kusema ni kuwa Lulu yuko katika hali nzuri,” alisema.
Sinza, mama mzazi wa Kanumba, Flora Mtegoa aliwasili juzi, ingawa mpaka jana alikuwa chini ya uangalizi wa madaktari baada kupata mshituko.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mazishi, Mtitu Game alisema hali ya mshituko imemfanya mama huyo kutokuwa na hali nzuri, hivyo kumfanya apewe matibabu nyumbani hapo ambako kikosi cha huduma ya kwanza kimeweka kambi.
Akizungumzia mvutano wa maziko ya msanii huyo, Mtitu alisema familia imekubaliana azikwe Dar es Salaam na pia baba yake, Charles Kanumba, alitarajiwa kuwasili jana kuhudhuria maziko.
Awali ulikuwapo utata wa kuhusu wapi azikwe Kanumba aliyezaliwa Januari 8, 1984 Shinyanga.
Wakati Kamati ya Maziko ikipendekeza azikwe kwenye makaburi ya Kinondoni, mama yake alitaka azikwe Bukoba huku baba yake akitaka azikwe Mwanza yaliko makazi ya babu yake aitwaye Steven Kanumba.
Naye Evance Ng’ingo anaripoti, kwamba jana Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliwafariji ndugu, jamaa na marafiki wa aliyekuwa msanii mahiri wa filamu nchini, Steven Kanumba na kuwataka wasanii kuendeleza harakati za Kanumba katika kusukuma gurudumu la sanaa nchini.
Pinda alisaini kitabu cha rambirambi na kuonana na mama wa marehemu aitwaye Flora Mutegoa na kumsihi awe mvumilivu wakati wa kipindi kigumu cha msiba.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki, alisema kuwa Pinda alimwagiza kuhakikisha kunakuwa na utaratibu mzuri wa matumizi ya barabara inayopita katika eneo la makaburi ya Kinondoni ambako msanii huyo atazikwa leo.
Alisema naye alimwagiza Mkuu wa Usalama Barabarani wa Mkoa wa Kinondoni ahakikishe barabara hiyo inatumika kwa njia moja kwa magari yanayotoka mjini kwenda Mwananyamala kwa Manyanya.
Pia alisema wanaotaka kutumia barabara hiyo kutoka Kwa Manyanya ikiwezekana wapite njia nyingine ili kuondoa usumbufu kwa wanaokwenda msibani. Mwenyekiti wa Kamati ya Mazishi, Mtitu Game, alisema Serikali imesimamia mahitaji yote muhimu ya leo.
Chanzo: Habarileo

1 comment:

Anonymous said...

Huyu mtoto anabalaa, she is too young for that. Damn life is is soo miserable sometimes. God be with u girl.