Monday, 9 April 2012

RATIBA YA MAZISHI YA STEVEN KANUMBA

Msanii wa filamu, aliyebeba mapenzi makubwa ya Watanzania, Waafrika na dunia kwa jumla, Steven Charles Kanumba aliyefikwa na mauti ghafla Aprili 7, 2012, atazikwa kesho Makaburi ya Kinondoni, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Mazishi ya Kanumba, yamepangwa na kuratibiwa kwa kuzingatia heshima, umaarufu, mapenzi yake kwa watu na hadhi ya kimataifa aliyonayo, hivyo imetolewa fursa ya wengi kumuaga msanii huyo ambaye ni mwanamapinduzi wa tasnia ya filamu ukanda wote wa Afrika Mashariki na Kati.

Mpangilio wa ratiba na nafasi itatolewa kwa kila mtu mwenye kuhitaji kushiriki mazishi ya Kanumba, kufanya hivyo katika tukio la kihistoria la kumsindikiza ndugu yetu huyo kwenye maisha ya milele. Hivyo, wito unatolewa kwa kila mtu kujitokeza kwenye shughuli nzima.

RATIBA
Mwili wa marehemu Steven Kanumba utachukuliwa kwa msafara kutoka Hospitali ya Taifa, Muhimbili saa 2:30 asubuhi. Utapitishwa Barabara ya Umoja wa Mataifa na Ali Hassan Mwinyi hadi Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni ambako Misa ya kumuombea itasomwa pamoja na salamu mbalimbali kabla ya watu wote kumuaga.
Wito unatolewa kwa watu kujitokeza kwa wingi kuanzia saa 2:00 asubuhi, wakijipanga kando ya Barabara za Umoja wa Mataifa na Ali Hassan Mwinyi ili wautolee heshima mwili wa Kanumba wakati ukitolewa Muhimbili kwenda Leaders Club.

Saa 3:30 asubuhi, mwili wa Kanumba utapokelewa Viwanja vya Leaders, ukitanguliwa na mapokezi ya wazazi wake, viongozi mbalimbali wa serikali ambao juu yao kabisa atakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohamed Gharib Bilal.
Saa 4:00, itakuwa ni muda wa kusoma Misa ambayo itachukua dakika 60, saa 5:00 kitakuwa kipindi cha salamu kutoka kwa watu mbalimbali.

Saa 6:00 mchana, ratiba ya kumuaga Kanumba itaanza mpaka saa 9:00 alasiri na baada ya hapo, utakuwa wakati wa kuusafirisha mwili kwa msafara kutoka Leaders Club mpaka Makaburi ya Kinondoni, msafara ukipita Barabara ya Tunisia, utakatisha Barabara ya Kinondoni kuelekea makaburini.

Saa 10:00 alasiri, mazishi yatafanyika kwa kufuata utaratibu wa imani ya marehemu.
Kamati ya Mazishi inatoa wito kwa watu watakaohudhuria shughuli ya kumzika ndugu yetu Kanumba, kuja na maua ili kumuaga kwa heshima.
Utulivu, unyenyekevu na ustahimilivu ni mambo muhimu yanayohitajika katika kipindi chote cha kumuaga mpendwa wetu Kanumba.

Bwana alitoa, Bwana ametwaa. Sisi wote tulimpenda kwa dhati na tulitamani aendelee kuwa nasi siku zote ila Mungu aliyemleta kwa mapenzi yake ameamua kumchukua. Jina lake lihimidiwe.

                                            K.N.Y GABRIEL MTITU
                                   MWENYEKITI WA KAMATI YA MAZISHI

No comments: