Sunday, 22 January 2012

WANAWAKE MALAWI WATISHIA KUANDAMANA

Mmoja wa wanawake akivuliwa nguo aina ya jeans
Takriban watu 3,000 wamekusanyika Blantyre nchini Malawi kupinga mashambulio dhidi ya wanawake wanaovaa suruali.
Baadhi ya wachuuzi wa kike wiki hii walipigwa na kuvuliwa nguo kwenye mitaa ya mji mkuu, Lilongwe, na Blantyre kwa kutovaa mavazi ya asili.
Rais Bingu wa Mutharika alisema kupitia redio ya taifa kuwa wanawake wana haki ya kuvaa wanachotaka.
Alikana taarifa kuwa aliamuru wanawake waache kuvaa suruali.
Mpaka mwaka 1994, wanawake kwenye nchi hiyo ya kusini mwa Afrika yenye misimamo mikali walikatazwa kuvaa suruali au sketi fupi chini ya uongozi wa kidikiteta wa Hastings Banda.
Wanaume pia walikatazwa kuwa na nywele ndefu.
Wanawake pia wameshambuliwa kwa kuvaa suruali katika nchi za Kenya, Afrika Kusini na Zimbabwe katika miaka ya hivi karibuni.

Mwandishi wa BBC aliyopo Blantyre Raphael Tenthani alisema makamu wa Rais Joyce Banda, waziri wa jinsia, wabunge kadhaa, wahadhiri wa chuo kikuu na wanaharakati walihudhuria maandamano ya Ijumaa.
Seodi White, mwanasheria na mwanaharakati wa haki za wanawake na aliyeandaa maandamano hayo, alisema wanawake hao hawakuvaa mavazi yasiyo ya heshima.
"Ndio Malawi ni nchi yenye msimamo mkali. Lakini tumekuwa tukivaa tunavyotaka, kwa kiwango cha heshima inayotakiwa, ambayo ni kiwango cha watu wote duniani, kwa miaka 18. Na hakuna anayeweza kusimama akasema ni kinyume na Wamalawi, " alikiambia kipindi cha Network Afrika cha BBC.
Alisema wanawake walikuwa wakilengwa na vijana ambao hawafurahishwi na hali ya kiuchumi nchini humo.
"Wachuuzi unaowaona mitaani si watu wazima. Hawa ni vijana, wadogo wa kuwa hata umri wa watoto wangu.
"Wananieleza mimi kuhusu utamaduni? Wananiambia mimi namna ya kuvaa?
"Hivi hili suala kweli ni kuhusu utamaduni au kitu kingine kinachohusiana na hali ngumu ya uchumi wanayokubaliana nayo watu wakitafuta namna ya kutoa hasira zao?
Awali, Bi Banda pia alilaumu mashambulio hayo kutokea kutokana na uchumi nchini Malawi, ambapo kwa sasa kuna upungufu mkubwa wa mafuta na fedha za kigeni.

No comments: