Monday 23 December 2013

Kauli ya uongozi wa Yanga dhidi ya wao

UONGOZI wa Yanga umemhakikishia kocha, Ernest Brandts, kwamba kibarua chake kipo salama, lakini kocha huyo ametaja mambo yaliyosababisha kikosi hicho kilichosheheni mastaa ghali kupata kipigo cha aibu kutoka kwa Simba katika mechi ya Mtani Jembe juzi Jumamosi.

Simba iliichapa Yanga kamili mabao 3-1, mabao ya Simba yalifungwa na Amissi Tambwe (mawili) na Awadh Juma, wakati Emmanuel Okwi ndiye aliyeifariji Yanga.
Brandts ambaye ni raia wa Uholanzi, aliliambia Mwanaspoti kwamba kimsingi kuna mambo manne yaliyochangia katika kupoteza mchezo huo, lakini kubwa ni wachezaji wa timu hiyo kujiona kila mmoja ni staa anayeweza kufanya jambo lolote.

“Tumefungwa ni kweli, hakuna atakayebisha juu hilo na uwezo tuliouonyesha, wachezaji wa Yanga sasa kila mmoja anajiona ni staa, hakuna aliyeko chini ya mwenzake. Hilo ni tatizo katika timu na ni kitu cha kwanza kilichochangia kufanya vibaya,” alisema.
“Jambo jingine ni kwamba, wapinzani wetu walicheza kitimu zaidi na walikuwa wakielewana na kuelekezana pale wanapokosea na walikuwa wepesi wa kumsaidia anayekosea, hawa walikaba pamoja na kupasiana pamoja.”

Alisema kikosi chake hakikucheza kitimu na ndiyo maana muda mwingi hawakuweza kutatua matatizo yaliyokuwa yakijitokeza uwanjani wala hawakuelekezana jambo la kufanya kwa wakati.
Kocha huyo pia alisema wachezaji wake kutoka timu za taifa walikuwa wamechoka na hawakucheza katika viwango vyao. Wachezaji hao ni Haruna Niyonzima (Rwanda), Emmanuel Okwi na Hamis Kiiza (Uganda) na Kelvin Yondani, Frank Domayo, Hassan Dilunga, Athuman Idd ‘Chuji’ na Mrisho Ngassa (Tanzania Bara).

Wachezaji wote hao walikuwa wakizichezea timu zao katika Kombe la Chalenji lililomalizika siku 10 zilizopita. Deo Munishi alikuwapo Chalenji lakini hakuchezeshwa mchezo huo.
Katika mechi ya Mtani Jembe, Simba ilicheza kitimu zaidi wakati viungo wakabaji wake; Jonas Mkude na Henry Joseph, walitawala kiungo huku Domayo na Chuji wakishindwa kuwadhibiti.
Kocha wa Simba, Zdravko Logarusic, alikuwa akiwaelekeza wachezaji wake kufinya uwanja kwa kucheza ndani zaidi wanaposhambulia na kuchomoka haraka kwenda pembeni hali iliyowachanganya mabeki wa pembeni wa Yanga, David Luhende na Mbuyu Twite.

Luhende alishindwa kumkaba Amissi Tambwe asifunge bao la kwanza kwani aliingia kati kukaba na alishindwa kumzuia haraka Ramadhan Singano ‘Messi’ hadi akamkwatua ndani ya eneo la hatari na kusababisha penalti iliyozaa bao la pili. Yanga walikuwa na mategemeo makubwa ya kushinda mchezo kutokana na kuwa na wachezaji wengi wazoefu akiwemo staa mpya, Emmanuel Okwi ambaye anasifika kwa kucheka na nyavu.

Source:Gazeti la Mwanaspoti.

No comments:

Post a Comment