Zanzibar.Vikosi vya Ulinzi na Usalama Zanzibar,
vimekamata kontena la futi 40 likiwa limepakia meno ya tembo
yaliyohifadhiwa kwenye mifuko ya nailoni yenye ujazo wa kilo 50,
yakisafirishwa nje ya nchi.
Meno hayo yalikamatwa Bandari ya Malindi majira ya
alasiri jana na polisi, Kikosi cha Kuzuia Magendo (KMKM), Maofisa wa
Usalama wa Taifa na raia wema waliotoa taarifa kuhusiana na mpango huo.
Akizungumza mjini hapa jana, Kamishna wa Polisi
Zanzibar, Mussa Ali Mussa alisema uchunguzi wa tukio hilo umeanza
ikiwamo kuwasaka wamiliki wa mzigo huo kupitia Kampuni ya Wakala wa
Kusafirisha Mzigo, iliyopewa kazi hiyo.
Kamishna Mussa alisema kazi ya kupakua mzigo na
kuchana gunia moja baada ya jingine tayari imeanza chini ya ulinzi mkali
wa askari ili kujua idadi ya meno na thamani yake. Alisema mzigo huo
ulikamatwa kupitia taarifa za siri zilizofanikisha kugundua kontena hilo
lililokuwa na meno hayo yaliyochanganywa na kuwekwa katikati ya makombe
(sea shells).
Naye Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis
Kagasheki alisema wakati umefika kwa Watanzania kushiriki na kuvikabili
vitendo vya ujangili vyenye lengo la kuangamiza wanyamapori hasa Tembo
na Faru.
Balozi Kagasheki alisema kazi inayofanywa na
askari ni sehemu ya utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili, huku
akiwapongeza askari kwa kufanikisha jukumu lao.
Naye Waziri wa Nchi , Ofisi ya Rais (Idara Maalumu
na Vikosi vya SMZ) Haji Omar Kheir alisema hakuna sheria za nyara za
Serikali kutokana na visiwa hivyo kutokuwa na wanyamapori wa aina hiyo,
lakini wahusika wanaweza kushtakiwa kwa kuhujumu uchumi ya Zanzibar
iliopitishwa mwaka huu.
CHANZO: GAZETI LA MWANANCHI
No comments:
Post a Comment