Thursday 8 August 2013

Raia wa kigeni anaswa akiiba kwenye ATM

Habari za kuaminika kutoka Bank of Africa (BOA) zinasema raia wa Bulgaria ambaye amekuwa akitafutwa kwa muda mrefu kwa kuhusika katika matukio ya wizi wa kwenye ATM amekamatwa akiwa katika jaribio la kuiba fedha katika Tawi la Afrikana, Kinondoni – Dar es Salaam.

Kuhusu tukio la jana, mmoja wa walinzi wa BOA aliyejitambulisha kwa jina moja la Frenky alisema mtuhumiwa huyo alipofika kwenye ATM hiyo aliingia na kuchukua fedha ambazo alizipeleka kwenye gari lake. Frenky alisema baada ya kupeleka fedha hizo, alirudi kwa mara ya pili ili achukue fedha nyingine ndipo walinzi hao walimkamata na kumfunga pingu.

Taarifa kutoka ndani ya Benki ya BoA zimetaarifu kuwa Benki hiyo imekuwa inapelekewa malalamiko na baadhi ya wateja kwamba wakienda kutoa fedha kwenye ATM wanakuta akaunti zao hazina salio wakati wanaamini zilikuwa na fedha. Hali hiyo ilipelekea BoA, pamoja na kuweka mitambo maalumu ya kutambua matukio yanayofanyika kwenye mashine za kutolea fedha pia wamewafundisha walinzi mbinu za kuwatambua wateja wanye mienendo inayotia mashaka.

Kwa mujibu mlinzi aliyeshiriki kumkamata mtuhumiwa huyo ni kwamba mtuhumiwa huyo alifika hapo Benki na gari lake saa 12 asubuhi. Aliingia kwenye ATM na kutoa fedha ambazo hazikujulikana ni shilingi ngapi na kuzipeleka kwenye gari lake, baadaye alirejea tena kwa ajili ya kutoa fedha zingine, wakati anaingia ndipo alipokamatwa.

Kamanda wa Polisi Kinondoni, Camilius Wambura alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa mtuhumiwa anashikiliwa na jeshi hilo huku uchunguzi dhidi yake ukiendelea.

CHANZO: dar24.com

No comments: