Sunday 21 July 2013

Mmiliki wa Home Shopping Center amwagiwa tindikali

Mfanyabiashara maarufu nchini, Said Mohamed Saad anayemiliki maduka ya vifaa vya nyumbani yajulikanayo kama "HOME SHOPPING CENTRE" amejeruhiwa usoni kwa kitu kinachodaiwa kuwa ni Tindikali.
Kutokana na tukio hilo, macho ya mfanyabiashara huyo yamedhurika vibaya mno ikiwa jicho moja ndilo limeathirika zaidi. Tukio hilo limethibitishwa na jeshi la polisi kupitia Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa DSM wilaya ya Kinondoni, Kamanda Yusuph Mrefu.

Akizungumza jana jijini DSM kamanda Mrefu alisema tukio hilo limetokea juzi usiku majira ya saa mbili usiku karibu na kambi ya Polisi Oysterbay. Alisema Mohamed alikumbwa na mkasa huo wakati akizungumza na wafanyakazi wake katika duka lake lililopo jengo la Msasani City Mall, Msasani jijini DSM.

"Siwezi kusema moja kwa moja kuwa ni tindikali au lah! kwa sababu wapo wataalamu wanaoweza kutambua kama ni tindikali au maji ya aina gani ambayo yamemdhuru"...alisema Kamanda Mrefu. Aliongeza kuwa, baada ya tukio hilo bilionea huyo alipelekwa katika hospitali ya Trauma kwa matibabu zaidi. Hata hiyo alisema hali yake si mbaya sana kwani baada ya tukio hilo aliweza kufika katika kituo cha polisi kilichopo jirani na kutoa taarifa. Alisema bado wanaendelea kumtafuta mhusika kutokana na Mohamed kutambua taswira ya mtu huyo aliyehusika na tukio hilo.

"Mtu huyo ambaye ni mwembamba mrefu alifika dukani kwake na kutoa kichupa kidogo mfukoni na kumwagia usoni, kisha kukimbia. kwahiyo upelelezi unaendelea kuhakikisha tunamkamata mtuhumiwa sahihi. Kazi ya kumsaka mtuhumiwa tena kwa kasi kubwa inaendelea..."aliongeza kamanda Mrefu.

CHANZO: HABARI LEO

No comments:

Post a Comment