Sunday 9 June 2013

Msanii wa bongo movie aliyeipeleka sanaa ya bongo ulaya

lucy-komba-1
Kama utakuwa shabiki na mtazamaji mzuri wa filamu za bongo movie, jina la Lucy Francis Komba halitakuwa jipya masikioni mwako.
Msanii huyu alianza sanaa katika Kundi la Kaole, akishiriki baadhi ya vipindi vya televisheni na baadaye kujiunga na Kikundi cha Dar Talent, ambapo alishiriki filamu moja ya vichekesho.
Katika sanaa, Lucy ameshacheza filamu zaidi ya 50 zikiwemo nne alizocheza nje ya nchi. Filamu ya kwanza aliyocheza nyota huyu na kuonyesha kipaji chake inafahamika kama Utata. Baadaye alishiriki filamu ya Yolanda, Division of Love, Jeraha la Ndoa, Talaka Wodini, Siri ya Moyo Wangu, Teke la Mama, Richmond, Swadakta na nyinginezo.
Kwa sasa Lucy ni mwigizaji wa filamu, mwongozaji, mtunzi wa stori na mtayarishaji wa filamu aliyefanikiwa kuvuka mipaka ya nchi hasa Bongo Movie akichanua hadi katika nchi za Burundi, Sierra Leone na Denmark.
Lucy kwa sasa anasubiri kuzindua filamu yake mpya aliyoichezea nchini Denmark.
”Nilienda kupumzika tu, lakini baada ya kuona wana mwitikio mzuri na filamu zetu, ilinibidi nicheze filamu niliyoipa jina la ‘Tanzania to Denmark’,” anasema Lucy.
Anabainisha kuwa filamu hiyo amecheza kwa gharama zake akishirikiana na Kampuni ya Vad Production ya Denmark inayojihusisha na uzalishaji wa filamu.
“Walinisaidia sana hadi hatua ya mwisho. Natarajia kuizindua mwezi huu wa Juni nchini Denmark, naamini itauza sana, maana nimecheza na wasanii maarufu wa huko,”anasema Lucy.
Aprili mwaka jana, msanii huyo alifanikiwa kwenda nchini Ghana kwa maandalizi ya kucheza filamu yake, hata hivyo hakuweza kufanikiwa baada ya msanii mwenzake Kanumba kufariki dunia.
“Mimi nilikuwa nimeshatangulia, nikiwa huko nikasikia amefariki ikanibidi nirudi kwanza nyumbani kwa mazishi yake,”anasema Lucy.

Kabla ya kuondoka Ghana, Lucy alibahatika kufanya mahojiano na mastaa wa nchini Sierra Leone waliokuwa wakikusanya washiriki wakubwa kwa lengo la kuandaa filamu itakayojitambulisha kimataifa.
Maandalizi hayo ni maarufu kama ‘famous film magazine in Africa’ ambayo imewashirikisha baadhi ya nyota akiwamo Van Vicker, Ini Edo, Desmond na wengineo katika kuandaa filamu ya ‘Repackage live’.
“Ilikuwa ni bahati tu,walivyoniona nikafanya nao mahojiano, basi nikafaulu movie yenyewe imeshakamilika na wana-plan ya kuifanyia uzinduzi kwenye nchi zote wanazotoka washiriki,”anasema Lucy.
Nje ya sanaa:
Nje ya tasnia ya filamu, Lucy ni mfanyakazi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akitumika kama Katibu Muhtasi katika Mahakama Kuu ya Tanzania, kazi aliyoifanya kwa kipindi kirefu sasa.
“Nilisomea kazi hiyo Chuo cha Utumishi wa Umma Magogoni Dar es Salaam. Maisha ya kazi na sanaa yanakwenda vizuri tu,”anaeleza.
Mbali na jukumu hilo, Lucy kwa sasa anashiriki mazoezi ya karate katika Viwanja vya Gymkhana kwa lengo la kujiweka fiti zaidi.
“Kwanza mchezo wa karate nilikuwa naupenda sana tangu nikiwa mdogo, najiweka vizuri ili pia kupambana na masuala ya unyanyasaji hasa kwa mtoto wa kike, ambayo yamezidi. Wanaume wakorofi hawatanisumbua,” anasema Lucy.
Mbali na hilo, anabainisha kuwa hatua hiyo pia inalenga kujiandaa kubadilisha mwelekeo filamu zilizozoeleka sasa.
Uhusiano wake:
Mitandao mingi na magazeti yamekuwa yakiripoti mitazamo tofauti kuhusu uhusiano wa mrembo huyu hata kufikia hatua ya mashabiki kukosa ukweli wake kwa sasa.
Baadhi ya mitandao imeeneza taarifa kuwa msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Tox Star kuwa ana uhusiano na Lucy, lakini taarifa hiyo inakanushwa na mwenyewe.
Lucy anasema kutokana na majukumu, nafasi na sanaa yake, jamii inaweza kuelezwa mambo mengi sana juu yake, lakini ukweli anaufahamu mwenyewe.
“Walianza kusema Mr Blue, wakasema sijui natoka na ........, sasa wanasema natoka Tox. Siyo kweli, yule ni mshkaji wangu tu, wote hao walikuwa wanapenda kucheza filamu na mimi, hivyo hata leo nikitoka na Pasha kwenye filamu watasema ni mpenzi wangu?,”anasema Lucy akihoji.
Historia yake:
Lucy alizaliwa Oktoba, 24 maeneo ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, alipata elimu ya awali na msingi Oysterbay, kabla ya kuendelea na Shule ya Sekondari Kibosho.
Binti huyo amesoma Chuo cha Utumishi wa Serikali, ambapo alisomea Teknolojia ya Mawasiliano na kupata Diploma.
Chanzo: Mwananchi 

No comments: