Thursday 8 September 2011

LIYUMBA AKUTWA NA SIMU GEREZANI

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi (DPA) wa Benki Kuu Tanzania (BoT), Amatus Liyumba ambaye anatumikia kifungo cha miaka miwili jela, ameingia matatani tena akidaiwa kukutwa na simu gerezani aliyoitumia kuwasiliana na Rais Jakaya Kikwete.
Liyumba kwa sasa anatumikia adhabu ya kifungo cha miaka miwili katika Gereza la Ukonga, baada ya kupatikana na hatia ya matumizi mabaya ya madaraka katika ofisi ya umma wakati wa akifanya kazi BoT.
Wakati bado akiwa anaendelea na adhabu hiyo, taarifa zilizopatikana jijini Dar es Salaam jana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile zilisema Liyumba alifikishwa katika Kituo cha Polisi cha Stakishari kilichopo Ukonga na kuhojiwa kwa kosa la kukutwa na simu gerezani.
Habari hizo zilifafanua kwamba Liyumba alifikishwa kituoni hapo saa 3:00 asubuhi kwa gari la Magereza lenye vioo vyeusi na kuhojiwa kwa muda wa takribani dakika 30 kuhusu tuhuma hizo.
Vyanzo hivyo vya habari vilifafanua kwamba, Liyumba anadaiwa kukutwa na simu ambayo ilibaki kituoni hapo kwa ushahidi.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, Julai mwaka huu Liyumba alimpigia simu Rais Kikwete kwa kutumia simu hiyo. Hata hivyo, bado haijafahamika ni nini hasa alichomweleza Rais lakini habari zaidi zinadai kuwa kitendo hicho kilimfanya mkuu huyo wa nchi kuhoji iweje Liyumba amiliki simu wakati ni mfungwa?
Kutokana na tukio hilo, inadaiwa kuwa maofisa usalama walimwekea mtego na juzi usiku walimdaka akiwa na simu hiyo na asubuhi yake walimpeleka kituoni hapo kwa mahojiano.
“Sasa hivi kinachofanyika ni uchunguzi katika Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) ili kujua alichokuwa akikifanya kwenye hiyo simu na uchunguzi huo ukikamilika basi anaweza kupandishwa kizimbani wakati wowote,”.

No comments: