Monday, 27 July 2015

Lowasa akaribishwa UKAWA rasmi

Kikao cha Kamati Kuu cha dharura cha Chama
Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
kilifanyika jana Kunduchi Beach Hotel kuanzia
saa mbili hadi saa tisa usiku. Jumla ya
wajumbe 36 walihudhuria kikao hicho
akiwemo Mwenyekiti Freeman Mbowe, Katibu
Mkuu, Dr Wilbroad Slaa nk. Aidha, Edward
Lowasa alihudhuria kama mwalikwa ambapo
aligharamia mkutano huo ikiwa ni pamoja na
gharama za ukumbi, chakula, nauli na posho
za wajumbe. Kiasi cha fedha alichotoa
Lowasa ni milioni 500 ambazo zimetumika
kwa matumizi niliyoyataja hapo juu.
Katika kikao hicho, mjadala mkubwa ulitawala
juu ya ujio wa Edward Lowasa ndani ya
CHADEMA na hatimaye kupeperusha bendera
ya chama hicho. Kutokana na tishio alilotoa
Mwasisi wa CHADEMA, Edwin Mtei juu ya
kuwafukuza Slaa na Lissu ikiwa hawatakubali
Lowasa awe mgombea Urais, wajumbe hao
waliamua kuridhia kwa shingo upande
maamuzi ya wenye CHAMA. Kutokana na hali
hiyo, Wajumbe wote 36 kwa kauli moja
waliridhia Lowasa kujiunga na CHADEMA na
awe Mgombea Urais.
Taarifa hii inahitimisha minong'ono iliyotanda
siku nyingi tangu Lowasa akatwe. Kutokana
na maamuzi hayo, uongozi wa CHADEMA
umepanga kumtambulisha rasmi Lowasa
kesho Jumanne Julai 28 kwenye Hotel ya
Kilimanjaro Kempisk iliyopo Dar es Salaam.
Hata hivyo, ni lazima tujiulize kwa nini
Lowasa anautaka sana urais kwa udi na
uvumba? Je ni kweli ana uchungu wa kutatua
kero zinazowakabili wananchi? Kama ndo
hivyo, kwa nini akiwa Waziri Mkuu hakutumia
nafasi hiyo na badala yake alitumia kufanya
ufisadi hali iliyopelekea kujiuzulu kwake
kutokana na kashfa za Richmond?
Ni vema tukatambua Watanzania kuwa
Lowasa huyu huyu aliyekataliwa na Mwalimu
Nyerere ndiye anayejiunga na CHADEMA. Ni
Lowasa huyu huyu aliyekataliwa na CCM
ndiye anayejiunga CHADEMA. Ni Lowasa huyu
huyu aliyesimama kwa tambo nyingi akisema
kuwa atakuwa wa mwisho kuondoka CCM na
watakaomkataa waondoke wao ndiye
anayejiunga na CHADEMA.
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyataja
mara kwa mara na kusisitiza kuwa ndiyo sifa
za Edward Ngoyai Lowasa kutofaa kuwa
kiongozi wa watu mambo yafuatayo;
1. Ni mtu mpenda mali na kujilimbikiza mali kwa
kiasi chochote na kwa hali yoyote
anayoiweza. Lowasa anamiliki mali ambazo
hazina maelezo ya jinsi alivyozipata. CCM
waliliona hilo na wakamfungashia virago.
2. Lowasa ni mtu dhaifu mbele ya mali na fedha
kwa sababu hiyo njia na nafasi yoyote iliyo
mbele yake anaweza kuitumia kupata fedha
zaidi na kujilimbukiza mali.
3. Ni mtu mwenye 'Pride' na kujitazama yeye tu
na kupenda kutambulika kwa mali aliyonayo.
Kwa sababu hiyo, anatumia muda na njia
nyingi kujijazia mali badala ya kuongoza na
kujali nchi yake (hii ndiyo sababu amekutwa
na kashfa lukuki za ufisadi na kubwa zaidi ni
ile ya Richmond iliyomfanya akaachia ngazi
nafasi ya Waziri Mkuu).
4. Lowasa anashindania zaidi kupata mali kwa
njia zozote, ziwe za halali ama haramu.
Kutokana na sababu hii ndio maana anajenga
chuki na kulipiza visasi kwa watu anaoona
kuwa vikwazo kwake katika kupata mali. Rejea
jinsi alivyotuhumiwa kushiriki kumtesa
Harrison Mwakyembe.
5. Lowasa huwajali zaidi matajiri kuliko watu wa
kipato cha chini. Hii ni kutokana na kulipa
fadhila kwa watu wanaomsaidia katika
harakati zake. Mathalan, wakati anatangaza
safari ya matumaini, Lowasa alikuwa
analazimisha wafanyabiashara kuchangia
harakati zake kwa ahadi ya kufanya biashara
na serikali akiwa Rais.
Kutokana na hoja hizi na nyingine nyingi bila
kusahau ugonjwa unaoendelea kumsulubu,
Lowasa hana sifa za hata kuteuliwa
kugombea Udiwani. CHADEMA wamehadaika
na tamaa ya fedha na wafuasi wa Lowasa.
Bilioni 10 alizohongwa Mbowe zimefanya
chama kitoke kwenye misingi yake na kuamua
kumpokea fisadi.
Nawahurumia sana Dr Slaa, Godbless Lema,
Tundu Lissu na wengineo ambao walijimaliza
kutaja madhaifu ya Lowasa akiwa CCM. Je
watafanya hivyo akiwa kwenye chama chao?
Tusubiri tuone.
Ila jambo moja tu napenda kuwahakikishia
wasomaji. Lowasa hana nafasi ya kushinda
Urais. Nasema haya kwa kujiamini.
Watanzania wamechoshwa na ufisadi.
Watanzania wamechoshwa na viongozi
wasiojali maslahi yao kama alivyo Lowasa.
Watanzania si wepesi wa kusahau.
Wameumizwa sana na hawa mafisadi na
mwaka 2015 ni wa kukata mizizi yote ya
ufisadi.

CHANZO: Mitandao ya kijamii

No comments: