POETRY

MOYO WANGU NI MCHANGA KUJIINGIZA PENZINI

Penzi hujengwa na vingi ingawaje sivioni.
Tabasamu tu halitoshi kuchekeana usoni.
Hisia zangu za ndani zinaishia kifuani.
Moyo wangu ni mchanga kujiingiza penzini. 

TUTOE HUMU GIZANI

Nchi yangu inaumwa na uchumi taabani.
Unapanda na kushuka kama bei mnadani.
Pesa haichenjiki elfu kumi kitu gani.
Ajira ota ndotoni wewe ndugu yako nani.
Ukabila ni kiini kuajiriwa kazini.
Dini ipo chinichini haisemwi hadharani.
Pesa yako bei gani ukae madarakani.
Uwezo wa kazi gani toa pesa mfukoni.
Siasa janja ya nyani ufisadi ndio fani.
Eeh mola wetu manani tutoe humu gizani.

MACHO YAKE YANASEMA

Macho yake yanasema, hakika ni mwenye huba.
Na ameshindwa kusema, moyoni yanamkaba.
Tena yeye mtu mwema,mwingi wa nyingi nasaba.
Usiku hauna wema, analala saa saba.
Na haishi kukusema, kwenye ndoto kwa mahaba.
Kesho sema nae vyema,mpunguzie shuluba.


NYODO KAMA VIFUNGO

Macho yako yenye wanja nayo ndefu yako shingo.
Umbo lako nane namba na huo mwendo  maringo.
Sauti kama kasuku na nyodo kama vifungo.
Amini mi nakupenda dhambi kusema uongo. 

MFANO KAMA HARIRI

Wangu kipenzi mzuri, mfano kama hariri.
Wewe kwangu ni habari, kifani chako dinari.
Zipite enzi dahari, ubaki wangu uturi.
Mola akujaze kheri, akuepushe na shari. 

KHERI YA MWAKA

Mshukuru mola wako kufika mwisho wa mwaka.
Jua si ujanja wako bali yeye alitaka.
Mtukuze mungu wako nenda katoe sadaka.
Mbili na kumi na mbili uwe mwaka baraka.
Nakutakia nafaka na pia kheri ya mwaka

JAPO NIOTE NDOTONI

Pendo lako sitopima, ratili uzito tani.
Huba zako zanikwama,nalemewa na uzani.
Hakika wewe ni mwema,mpenzi wangu mwandani.
 Kheri ya usiku mwema,japo niote ndotoni.

ZIJE MVUA NA JUA

Kwako nimepata penzi moto zaidi ya jua.
Kazi za nje sizitaki naogopa kuugua.
Kwako tuli nimeridhi wengine wote pangua.
Daima dawamu nawe zije mvua na jua

KIDONDA CHANGU MWENYEWE

Kidonda changu mwenyewe siwezi kuziba pua.
Japo chanipa kiwewe kikiunguzwa na jua.
Tena kiwewe cha mwewe kikipatwa na mvua.
Kidonda changu mwenyewe ntakiombea dua.

MGOMBA NI MTI AU UA?

Mgomba wanipa shaka ni mti au ni ua.
Na tena unatumika sherehe kuzipambia.
Ukizaa naukata na hauwezi kukua.
Kama ungekuwa mti tanuri ningechimbia.
Ili nichome mkaa uchumi kujikwamua.
Wala hauna matawi niweze kuning'inia.
Mbona ndizi unazaa Kama mgomba ni ua.
Tena bila ya msimu tunda unajizalia.
Hakika wanitatiza maswali kunijazia.
Waungwana nijuzeni majibu kunipatia.
Eti mgomba ni mti au mgomba ni ua?

KITAMBI KIMENIPONZA

Kitambi kimeniponza,sina hamu asilani.
kimenifanya nawaza maisha si  ya thamani.
Mahari mara ya kwanza natakiwa milioni.
Wakashindwa kunioza kwa laki tano jamani.
Nikampenda shariza asili ya arabuni.
Ile tu kumposa dhahabu za milioni.
Ni kitambi sina pesa mi kabwela kama nini.
Kitambi kinaniponza nakosa mke jamani. 

ZILE SUNGURA NA FISI

Zile sungura na fisi, hadithi nilishaacha.
Tena kwangu ni najisi, na ndoto za alnacha.
Mapenzi ya yangu nafsi, kwako siwezi kuficha.
Sipokuona najihisi,kidole bila ya kucha.
Pendo lako makhususi,ni mwanga kila kukicha.
KWA MASHAIRI ZAIDI BOFYA HAPA MASHAIRI.